Tuesday 14 July 2015

UKAWA, TANZANIA.




UPATIKANAJI wa mgombea mmoja wa urais kupitia vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), umeendelea kujadiliwa katika kikao cha siri cha vyama hivyo, huku hali ikijionesha kuwepo kwa mvutano baina ya vyama vikuu katika umoja huo.
Jana baadhi ya vyombo vya habari vilidai kuwa umoja huo, unaoundwa na Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, ulishaafiki Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa, ndio apeperushe bendera ya vyama hivyo na kwamba uamuzi huo ungetangazwa jana.
Lakini umoja huo ulikutana kwa ajili ya kujadiliana na kutoa tamko juu ya makubaliano yao ya ugawanaji wa majimbo na mgombea rais atakayesimamishwa tangu saa nane mchana mpaka saa mbili usiku bila kutoa tamko lolote.
Mkutano huo uliofanyika katika jengo jipya la Kisenga LAPF liliopo Kijitonyama ambako waandishi walipiga kambi, lionekana kukumbwa na sintofahamu kwa wanahabari ambao walikaa zaidi saa tano kusubiri kile kitakachoamuliwa na umoja huo.
Hata hivyo baadhi ya wajumbe wa mkutano huo akiwemo Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) walitoka mapema kabla ya kikao hicho kumalizika hali iliyozua maswali zaidi.
Alipohojiwa na waandishi wa habari kuhusu kutoka katika mkutano huo na kuacha ukiendelea, Kafulila alisema bado hawajafikia uamuzi ila watakachoafikiana kitatangazwa na viongozi wa umoja huo na si yeye kwa kuwa hana mamlaka ya kusemea viongozi wa umoja huo.
Viongozi wa umoja huo waliohudhuria mkutano huo ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wake, Dk Willbrod Slaa, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmauel Makaidi na Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe.

No comments:

Post a Comment