Monday 13 July 2015

SIASA TANZANIA.

DAKTARI wa Kemia, John Pombe Joseph Magufuli (56) ndiye mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
Waziri huyo wa Ujenzi aliwashinda wagombea wenzake wawili, Balozi Amina Salum Ali na Dk Asha-Rose Migiro kupata uteuzi huo wa CCM.
Alishinda katika Mkutano Mkuu Maalumu uliofanyika juzi na jana kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Dodoma (DCC) eneo la Makulu katika Makao Makuu ya Tanzania, Dodoma.
Mbunge huyo wa Chato katika Mkoa wa Geita, alipata kura 2,104 kati ya kura halali 2,416 zilizopigwa na wajumbe 2,422 wa mkutano huo. Ushindi wake kwa mujibu wa Spika wa Bunge, Anne Makinda ni asilimia 87.1, huku wenzake, Balozi Amina akipata kura 253 (asilimia 10.5) na Dk Migiro kura 59 (asilimia 2.4).
Hii ni mara ya kwanza kwa wanawake kufika hatua ya tatu bora katika mchakato wa kumpata mgombea wa urais ndani ya CCM. Makinda aliyekuwa miongoni mwa jopo la kuhesabu kura hizo, alisema kura sita ziliharibika wakati alipotangaza matokeo jana saa 6.50 mchana.
Wakati akitangaza matokeo hayo, Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Kikwete alimtaka kusoma polepole matokeo hayo kwa wajumbe waliokuwa wakimsikiliza kwa makini. Wagombea hao watatu walipigiwa kura juzi usiku baada ya kuteuliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa kwa kupigiwa kura miongoni mwa wagombea watano waliopitishwa na Kamati Kuu ya CCM.
Dk Magufuli aliongoza akifuatiwa na Balozi Amina, Dk Migiro, na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambao kura hazikutosha.
Dalili njema kwa Dk Magufuli kushinda uteuzi huo, zilionekana tangu juzi usiku wakati akiingia katika ukumbi wa mkutano, alishangiliwa mno na wajumbe hao na kuzunguka kila kona kuwasalimu.
Alilazimishwa na Katibu wa NEC wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye kurudi katika eneo lake kwenye mkoa wake wa Geita kukaa, ili kuruhusu mkutano huo uendelee kwa utulivu. Jana, baada ya kutangazwa mshindi, aliitwa mbele ya meza kuu na Rais Kikwete, na alipanda eneo hilo saa 12.58 mchana na dakika mbili baadaye alifika kwa Rais Kikwete, wakakumbatiana na kisha akainuliwa mkono kutambulishwa kwa wajumbe.
Ilipotimu saa 7.05, bendi ya Tanzania One Theatre (TOT), ikimkosa kiongozi wake mahiri, Kapteni John Komba aliyefariki dunia mapema mwaka huu, iliongoza kuimba wimbo maarufu wa “Sasa Kumekucha, Jogoo ameshawika Dodoma.”
Baadaye, mkewe Dk Magufuli, Janeth alipanda katika meza kuu na muda mfupi baadaye, mke wa Rais, Mama Salma Kikwete aliungana naye hapo, na sherehe zikaendelea hadi Kamati Kuu ilipokwenda kushauriana kuhusu jina la Mgombea Mwenza.
Kwa ushindi wake, Dk Magufuli anasubiri baraka za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuidhinisha jina lake ili apeperushe bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu. Atapambana na vyama vya upinzani vinavyojiandaa kusimamisha mgombea mmoja chini ya mwavuli wa kinachoitwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Aidha, Dk Magufuli mwenye Shahada ya Uzamivu ya Kemia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anajiandaa kurithi mikoba ya Rais Kikwete endapo atashinda uchaguzi huo na kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano.
Mbali ya kuwa Waziri wa Ujenzi kuanzia mwaka 2010 hadi sasa, Dk Magufuli aliyezaliwa Oktoba 29, 1959 wilayani Chato, amewahi kuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, zote katika Serikali ya Rais Kikwete.
Katika Awamu ya Tatu, alikuwa Waziri wa Ujenzi kuanzia mwaka 2000 hadi 2005 na Naibu Waziri wa wizara hiyo kuanzia 1995 hadi 2000. Alipopewa fursa ya kuzungumza na wajumbe wenzake wa Mkutano Mkuu Maalumu, Dk Magufuli alisema, “Nimehemewa sana.”
Alisema jana ilikuwa siku muhimu sana katika historia ya chama hicho na kwake mwenyewe. “Jana (juzi) nilisema nitumieni nami nitawatumikia, nawashukuru kwa kura za kishindo, sina cha kuwalipa isipokuwa nasema ‘asanteni sana, sana, sana.”
Aliahidi kuwatumikia wanaCCM na Watanzania kwa ujumla kwa nguvu zake zote, uwezo wake na vipaji vyote alivyopewa na Mwenyezi Mungu katika kuongoza baada ya kupewa heshima hiyo kubwa. Alisema CCM ni moja na wanaCCM ni wamoja, hivyo anatarajia kufasiri kauli hiyo kuwa ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu ujao.
“Tudhihirishe kwa vitendo kuwa Umoja ni Ushindi. Wenzangu 38, viongozi, wanachama na mashabiki wa chama chetu tuungane pamoja ili ushindi wa chama chetu uwe mkubwa,” alifafanua.
Alisema uimara wa chama, uongozi imara na madhubuti na hamasa ya juu, pamoja na sera zake, ndio umeifanya CCM iwe na heshima ndani na nje ya nchi, na kwa kufuata taratibu za demokrasia ndani ya chama, inaonesha ni chama kilichokamaa. “Mtandao wetu wa ushindi ni mmoja. Nitafanya kila jitihada kuzitetea, kuzifafanua na kuzilinda sera hizi nzuri.
Asanteni kwa mchakato huu. “Niwathibitishie kwamba nitakuwa nanyi kweli kweli, nitakuwa mtumishi wenu,” alisema Dk Magufuli na kuongeza kuwa mchakato wa uteuzi wake ulikwenda vizuri na wagombea wenzake wote 38 wanaungana pamoja.

No comments:

Post a Comment