Monday 13 July 2015

SIASA TANZANIA.

 BARAZA la Ushauri la Chama Cha Mapinduzi (CCM), lenye wajumbe wazee wenye uzoefu, jana lilizima hoja kinzani ndani ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ambazo zilikuwa zinataka kurejeshwa kwa jina la Edward Lowassa katika kuwania uteuzi wa urais.
Waziri Mkuu wa zamani, Lowassa ni miongoni mwa wanachama 33 wa CCM waliochujwa na Kamati Kuu usiku wa kuamkia jana.
Lakini kukatwa kwa jina la Lowassa, kulizua maneno na sintofahamu miongoni mwa wajumbe wa NEC na walionesha fadhaa yao wakati wa ufunguzi wa kikao walipoimba wimbo wa “Tuna imani na Lowassa,” wakati wakuu wa CCM na viongozi wastaafu walipoingia kikaoni.
Lakini wakati wa kikao hicho ambacho waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuingia, chanzo chetu kimeeleza kuwa wazee hao walituliza mambo wakisisitiza Katiba ya CCM na maslahi ya chama, ni muhimu kuliko maslahi binafsi au kingine chochote kile.
Wazee
Miongoni mwa waliozungumza ni marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa.
Wengine ni Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM John Malecela, na wabunge Christopher ole Sendeka na Livingstone Lusinde ‘Kibajaji.”
Wote katika hoja zao waliunga mkono uamuzi wa kumchuja Lowassa na kutetea maslahi mapana ya Chama na Katiba ya chama hicho kikongwe.
Malecela ambaye amerejea nchini juzi akitokea London kwa matibabu, alisikika akisema CCM ni muhimu zaidi kuliko mtu yeyote na kwamba kama kuna mtu anajiona ni muhimu zaidi, atoke.
Karume katika mchango wake, alieleza kuwa ni muhimu kuwa na mapenzi yasiyopitiliza kwa baadhi ya wanachama wenzao.
Mzee Mwinyi, Karume, Mkapa na Malecela, Pius Msekwa pamoja na Dk Salmin Amour Juma ambaye ni mgonjwa, wanaunda Baraza la Ushauri la Wazee wa CCM, lililoundwa miaka ya karibuni.
Wote hao isipokuwa Dk Salmin walihudhuria kikao cha Kamati Kuu juzi usiku pamoja na NEC jana na michango yao ndiyo iliyosaidia kwa kiasi kikubwa wajumbe kukubaliana na uteuzi wa CC.
Sendeka kwa upande wake, alieleza kuwa hali inayotokea sasa ni kutokana na kukiukwa kwa misingi ya chama hicho na kwamba kimeingiliwa na baadhi ya watu ambao wanataka kukivuruga.
Lusinde alisikika akisema kuwa mvutano uliotokea kwa wanachama hao ni kuwa baadhi yao wanatumiwa na wamehongwa fedha.
Kutokana na hali hiyo, NEC hatimaye ilikubaliana na uamuzi wa CCM wa kumchuja Lowassa, ambaye amechujwa pamoja na majina mengine makubwa yakiwamo ya Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Mtafaruku asubuhi
Awali, asubuhi baadhi ya wafuasi wa Lowassa walipaza sauti wakisema hawakubaliani na uteuzi wa CC na kudai kuwa watafanya mabadiliko makubwa ndani ya NEC, jambo lililoshindikana.Kwa uamuzi wa NEC, majina matano yaliyotoka CC yalipigiwa kura kuanzia saa 10.45 jioni.
Katibu wa NEC wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, aliwaambia waandishi wa habari saa 10.50 jioni kuwa kikao kimeisha na wajumbe wanaendelea kupiga kura kwa majina yale yale, akimaanisha aliyoyatangaza mapema asubuhi.
Waliopigiwa kura ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe, Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli na Waziri wa Katiba na Sheria Dk Asha-Rose Migiro.
Wengine ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Balozi wa Umoja wa Afrika (AU) katika Marekani, Amina Salum Ali.
Upigaji kura huo utachuja majina ya wagombea hao na kubaki matatu ambayo yalitarajiwa kupigiwa kura katika Mkutano Mkuu wa CCM, uliotarajiwa kuanza jana saa tatu usiku.
Aidha, Balozi Amina aliwasili ukumbini hapo baada ya upigaji kura kuanza akifuatana na mmoja wa watu wake wa karibu, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa UWT, Halima Mamuya.
Balozi Amina na Dk Magufuli si wajumbe wa NEC, lakini kwa muda mrefu, Waziri huyo wa Ujenzi alikuwa katika jengo la White House na kabla ya kuanza kwa kikao cha NEC, alikuwa akiomba kura.
Pia ilielezwa kuwa Lowassa alikuwa abaki ndani baada ya kuitwa kuzungumza na Wazee baada ya kikao cha NEC, huku mitandao ya kijamii jana ikimhusisha na kukihama chama hicho tawala.
Baadae kikao cha NEC kilipitisha majina matatu ambayo yalifikishwa katika Mkutano Mkuu kumpata mgombea wa Urais kupitia tiketi ya CCM. Waliopitishwa ni Dk John Magufuli, Balozi Amina Salum Ali na Dk Asha-Rose Migiro.

No comments:

Post a Comment