Saturday 11 July 2015

CCM WAKESHA






HALMASHAURI Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM inatarajiwa kukutana leo, kupigia kura majina ya wanachama wake watakaopelekwa katika Mkutano Mkuu ili kupata mgombea wa urais.
NEC inatarajiwa kukutana katika Makao Makuu ya chama hicho, White House, katika Barabara ya Nyerere mjini hapa, kulingana na ratiba ya vikao vya uteuzi vya chama hicho tawala nchini.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, juzi Jumatano kulitarajiwa kufanyika kikao cha Kamati ya Maadili na Usalama na jana Kamati Kuu (CC) ilitarajiwa kukaa katika mwendelezo wa vikao vya uteuzi.
Hata hivyo, kikao cha Kamati ya Maadili na Usalama hakikufanyika juzi kama ilivyotarajiwa, na hakukuwa na sababu zilizowekwa bayana kuhusu kutofanyika kwa kikao hicho.
Aidha, Kamati Kuu ambayo ilipangwa kufanyika jana, hadi saa 2 usiku, ilikuwa haijaanza kikao.
Kulikuwa na taarifa za kutofanyika kwa kikao hicho jana, na Katibu wa NEC wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alipoulizwa kama kikao hicho hakitafanyika, alisema wanasubiri kauli ya Mwenyekiti wa Taifa, Rais Jakaya Kikwete.
Jana, Rais Kikwete alikuwa na ratiba mbili kubwa; asubuhi alifungua rasmi jengo la Ukumbi wa Mikutano wa CCM uliojengwa eneo la Makulu mjini hapa ambao utatumika kwa Mkutano Mkuu uliopangwa kufanyika kesho na keshokutwa.
Aidha, jioni Rais Kikwete alilihutubia Bunge ikiwa ni kutekeleza matakwa ya kisheria ya kumaliza uhai wa Bunge la 10 lililoanza mwaka 2010.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wajumbe wa CC walieleza kuwa uwezekano wa vikao hivyo kufanyika jana usiku, ulikuwa mdogo.
Badala yake, mjumbe mmoja wa Kamati Kuu alisema “ngoma (shughuli) yote itakuwa kesho (leo) kuanzia kikao cha Maadili, Kamati Kuu na kisha Halmashauri Kuu. Kama ni majina basi mtayapata kesho (leo).”
Kamati Kuu inatarajiwa kuchuja majina ya wagombea hao 42 wa urais katika CCM na kupeleka majina matano katika NEC, ambayo yatapigiwa kura na kupata matatu ya kwenda Mkutano Mkuu.
Hata hivyo kati ya idadi hiyo ya waliochukua fomu, 38 ndiyo waliorudisha fomu.
Tayari mji wa Dodoma umefurika wajumbe wa vikao hivyo na wale wa Mkutano Mkuu waliingia kwa wingi katika mji huu wa Makao Makuu ya nchi kuanzia jana asubuhi, tayari kusaka mrithi wa Rais Kikwete aliyeingia madarakani mwaka 2005.
Rais Kikwete anamaliza muda wake kikatiba mwaka huu na Uchaguzi Mkuu utafanyika Oktoba 25, 2015.
Dodoma tulivu Hadi jana hali mjini hapa iliendelea kuwa tulivu huku viongozi wa juu wa chama hicho, wakihudhuria shughuli zilizokuwa zikifanywa na Mwenyekiti Rais Kikwete.
Kwenye Jengo la Makao Makuu ya chama hicho hali ilikuwa tulivu huku shughuli za maandalizi ya Mkutano wa NEC na Mkutano Mkuu ambao huchukua idadi kubwa ya wajumbe wa CCM , yakiendelea kwa kuandaliwa vitambulisho na vibao vya kutambulisha wajumbe wa mikutano hiyo.
Moshi mweupe
Wakati jina la atakayepeperusha bendera ya CCM katika kinyang’anyiro likisubiriwa kwa shauku kubwa nchini, mjadala na taarifa zisizo rasmi juu ya vikao vya chama hicho tawala, zimekuwa zikivuma katika mitandao ya kijamii na vijiwe.
Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, Nape alisisitiza kwamba, CCM haitachagua mgombea wa kiti cha urais kwa presha za wapambe wa wagombea.
Nape alisisitiza kwamba chama kina kanuni na taratibu, ambazo zitafuatwa kwa ajili ya kupata mgombea.

No comments:

Post a Comment