Friday 31 July 2015

BVR DAR

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeongeza siku nne zaidi kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa Mfumo wa Kielektroniki (BVR).
Kwa ratiba iliyotolewa awali na NEC, leo ndio ilikuwa siku ya mwisho kwa wakazi wa jiji hilo kubwa nchini, kujiandikisha kwenye daftari hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema wameongeza siku hizo kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi ulioonekana katika vituo mbalimbali vya kujiandikisha.
Alisema uandikishaji huo kwa nchi nzima ulianza Februari 23, mwaka huu mkoani Njombe na mpaka Julai 29, takwimu zinaonesha jumla ya wananchi 18,826,718 wameandikishwa huku lengo likiwa ni kuandikisha wananchi milioni 23.
Aliongeza kuwa kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza, ikiwemo ya mashine, Tume iliweza kuongeza mashine ili kuharakisha kazi hiyo kwa Jiji la Dar es Salaam.
“Tulianza na mashine 250 tu, baada ya uandikishaji kwa mkoa wa Njombe tuliendelea kuongeza mashine na mpaka sasa tuna mashine 8,000 ambazo tuna uhakika zitafanikiwa kukamilisha uandikishaji kwa siku zilizobakia,” alisema Lubuva.
Pia, alisema ili kuhakikisha kila mtu anajiandikisha vizuri na kuandika kumbukumbu sahihi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi itaonesha majina ya wananchi waliojiandikisha na taarifa zao ili kila mtu aangalie kama kumbukumbu zake zipo sahihi.
“Tumeamua kuonesha daftari hili na tutaanza Agosti Mosi katika mikoa ambayo tayari wamekamilisha uandikishaji na endapo kutakuwa na tatizo lolote lifanyiwe marekebisho na kila mtu atambue alipojiandikisha ili aweze kupata nafasi ya kupiga kura,” Lubuva alisema.
Aidha, alisema suala la kujiandikisha kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, si la NEC, bali ni la Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambayo inapaswa kupanga utaratibu na ratiba kuwawezesha wanafunzi hao, kujiandikisha katika eneo ambalo atakuwepo ifikapo Oktoba 25.
“Suala la wanafunzi kujiandikisha naona sasa hivi linachukuliwa kisiasa. Kila mwanafunzi anapaswa kujiandikisha mahali atakapokuwa Oktoba 25 na si jukumu letu kujua ni wapi mwanafunzi atakuwepo, kila mmoja ni mtu mzima na anapaswa kujiandikisha,” alisema Lubuva.
Pia, alisema kuhusu sula la wahamiaji kujiandikisha, kila mwananchi anapaswa kumtambua mwenzake ili kuepuka kumuandikisha mtu ambaye si Mtanzania.
“Mkituachia Tume peke yetu, kwakweli hatutaweza na ndio maana katika vituo kuna mawakala ambao wanapaswa kutambua yupi ni mkazi na yupi anazamia,” alisema Mwenyekiti huyo wa NEC.
Wakizungumzia hatua hiyo ya NEC ya kuongeza siku nne zaidi za kujiandikisha, wananchi wengi waliozungumza na gazeti hili, walilalamikia hatua hiyo wakisema siku nne zilizoongezwa ni chache na ni vigumu watu wote kupata nafasi.
Hamidu Baruani, mkazi wa Majohe wilayani Ilala, aliliambia gazeti hili kuwa siku zilizoongezwa bado ni chache, ukizingatia kuwa watu wengi bado hawajaandikishwa.
Aliongeza kuwa kumekuwepo na uhaba wa mashine na waandikishaji wamekuwa wanaandikisha watu kwa taratibu, hatua inayolazimu baadhi ya watu kulala vituoni, wakisubiri kuandikishwa bila mafanikio.
“Siku ni chache, kwa kweli kama mimi nilikaa sana kwenye kituo na nyumbani kwangu nilitoka saa nane usiku, kitendo ambacho pamoja na changamoto nyingine pia kilihatarisha maisha yangu,” alisema Baruani.
Aidha, Moses John mkazi wa Yombo wilayani Ilala, alisema kumekuwa na vurugu katika maeneo ya kujiandikisha, kitendo kinachosababisha watu wengi kushindwa kujiandikisha. “Mimi sijafanikiwa kujiandikisha, kila nikifika fujo tu watu ni wengi, ila naamini katika siku hizi zilizoongezwa, nitafanikiwa kujiandikisha japo siku hizo bado ni chache,” alisema John.
Kwa upande mwingine, NEC imewashukuru wananchi wa Dar es Salaam kwa kuwa wavumilivu wakati wa uandikishaji na wametakiwa kuendelea kutoa ushirikiano ili kufanikisha uandikishaji huo.

No comments:

Post a Comment