Thursday, 9 July 2015

SIASA, DODOMA.





Joto limepanda mjini hapa, ambapo mchujo wa kumpata mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), unaanza rasmi leo, pale Kamati Kuu (CC) itakapochuja majina ya watangaza nia 38 waliochukua na kurejesha fomu na kubakiza watano.
Kamati Kuu itachuja majina ya watangaza nia hao huku ikizingatia kile kilichochambuliwa na kupendekezwa na Kamati ya Ushauri ya CCM, inayoundwa na wazee wastaafu, iliyokutana hivi karibuni na pia Kamati ya Nidhamu na Usalama, iliyokutana kwa siku nzima jana chini ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete.
Kamati ya Maadili na Usalama iliyokutana jana, ilihusisha wajumbe kutoka CCM na serikalini wakiwemo watendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Idara ya Usalama wa Taifa.
Rais Kikwete aliwasili mjini hapa saa 8 mchana jana na kuungana na wajumbe wa Kamati ya Maadili na Usalama katika kikao kilichofanyika Ukumbi wa White House, uliopo ndani ya Jengo la Makao Makuu ya CCM.
Awali wanaCCM 42 walijitokeza kuchukua fomu za kuwania kuteuliwa kugombea urais kupitia chama hicho. Lakini, hadi ilipofika tarehe ya mwisho ya urejeshwaji wa fomu, wanaCCM wanne walishindwa kurejesha fomu na kupoteza sifa.
Wakati Kamati Kuu itafanya kazi ya kuchuja majina ya watangaza nia hao kubakia watano, watakaofikishwa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) kesho.
Jana kazi iliyofanywa na Kamati ya Maadili na Usalama, ilikuwa ni kupitia sifa za watangaza nia hao kwa kuzingatia vigezo zaidi ya 10 vilivyowekwa na chama hicho.
Vigezo Vigezo hivyo vilivyozingatiwa ni uwezo mkubwa na uzoefu kwenye uongozi; Uadilifu; Unyenyekevu na busara; Elimu ya chuo kikuu, upeo mkubwa wa kuimarisha na kulinda muungano, umoja na amani, upeo mkubwa katika masuala ya kimataifa.
Vingine ni kwamba, mgombea asiwe na hulka ya udikteta; awe tayari kulinda kanuni, sheria na utawala bora; awe mtetezi wa wanyonge na haki za binadamu; asiwe na tamaa ya kujipatia umaarufu; awe tayari kuzifahamu kuzitetea na sera na ilani ya CCM; awe ni mpenda haki kwa maana kwamba awe tayari kupambana na dhuluma.
Vigezo vingine vilivyotumika ni mgombea asiwe mtu anayetumia uongozi kujilimbikizia mali; awe ni mtu makini na anayezingatia masuala ya uongozi.
Hata hivyo, kama ilivyokuwa kwa kikao cha Wazee Washauri wa CCM waliokutana hivi karibuni, pia mambo yaliyojadiliwa kwenye kikao cha Maadili na Usalama hayakuwekwa wazi mbele ya waandishi wa habari, waliokusanyika nje ya jengo kutwa nzima jana.
Kuwasili kwa Rais Kikwete mjini hapa jana, kunamfanya kuwa kiongozi wa juu wa vikao vyote vya chama hicho hadi pale atakapopatikana mgombea urais kupitia CCM.
Kwa nafasi yake ya uenyekiti wa Taifa, Rais Kikwete huongoza vikao vya Kamati Kuu, NEC na Mkutano Mkuu utakaofanyika Julai 11 na 12. Mchujo watatu Kazi ya NEC kesho itakuwa ni kuchuja majina kutoka matano hadi matatu, ambayo yatawasilishwa kwenye Mkutano Mkuu, ambao utachuja na kupitisha jina moja la mwanaCCM, atakayebeba bendera ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
CCM yapewa angalizo Katika hatua nyingine, Kamati ya Maadili na Usalama na Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimetakiwa kutenda haki na kupitisha jina la mgombea urais wa chama hicho, atakayesimamia misingi ya umoja, haki, mshikamano na uadilifu.
Wajumbe wa kamati hizo wametakiwa kuwa makini, kuhakikisha uteuzi wao unakuwa ni wa haki, ikisisitizwa kwamba chama hicho ni taasisi kubwa, hivyo kusipokuwa na umakini kutasababisha mgawanyiko.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba wakati akizungumza kwenye Kongamano la Amani na Umoja, lililofanyika jijini Dar es Salaam jana, ambapo alisema misingi hiyo ndiyo itasaidia kudumisha amani na utulivu nchini.
Alisema wakati huu ambao nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu Oktoba, vipo viashiria vingi vya uvunjifu wa amani vinajitokeza, hivyo wajumbe wachague viongozi watakaosimamia misingi ya amani. Alitaja baadhi ya viashiria hivyo kuwa ni udini, ukabila, ukanda na uchama, ambapo kama visipodhibitiwa hali hiyo inaweza kuhatarisha amani ya nchi.
“Mpaka sasa kuna watu zaidi ya 38 ambao wamechukua fomu ya kuwania urais, wakati kamati hizo zitakaa muda mfupi kufanya uteuzi huo, hivyo basi wanapaswa kutuliza vichwa vyao na kuhakikisha kuwa mtu wanayemchagua anakuja kusikiliza matatizo ya wananchi na kusimamia misingi hiyo,” alisema.
Alisema tatizo lililojitokeza kwa wagombea hao ni kwamba kila mmoja amekuja na ahadi zake, wakati chama kina Ilani yake, jambo ambalo linawafanya wajumbe wa kamati hizo, kuumiza vichwa kwa kupitia wasifu wa wagombea hao na kufanya uamuzi.
“Baadhi ya wagombea wanatoa matamshi mazuri ili waweze kupata nafasi hiyo, lakini matamshi yao yanaonekana ni njia ya kutafuta kuchaguliwa na wakichaguliwa watafanya mambo yao bila kuangalia maslahi ya wananchi,” alisema Jaji Warioba.
Watumia rushwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku alisema rushwa ni miongoni mwa mambo yanayorudisha nyuma maendeleo ya taifa, jambo ambalo wananchi hawana budi kuitakaa.
Alisema rushwa ni adui wa haki, hivyo watu wanaotafuta uongozi kwa kutumia rushwa ni wabaya kwani wanaweza kuhatarisha mani ya nchi. Butiku alishutumu kitendo cha baadhi ya wagombea kununua watu wenye uamuzi.
Alisema kitendo cha kununua vyombo vya habari, kinachangia kupotoshwa kwa taarifa, hali ambayo vyombo hivyo vinaweza kuchangia uvunjifu wa amani.
Ubinafsi wa Ukawa Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole alisema vyama vya siasa havina budi kuondoa ubinafsi, vinginevyo watavunja misingi ya demokrasia.
Alisema hata vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vina ubinafsi hivyo visipozingatia hilo vitadhoofisha misingi ya demokrasia. “Ukawa wana ubinafsi ambao utasababisha kuondoa misingi ya utaifa na demokrasia, hivyo basi wanapaswa kujirekebisha na kujenga misingi ya umoja na mshikamano,”alisema Polepole.
Aidha, alishauri Kamati ya Maadili ya CCM kuwakata wagombea wenye dosari, wasiweze kupewa nafasi za uongozi bila ya kufanya hivyo atashirikiana na viongozi wengine kuhamasisha wasichaguliwe.
Jaji Manento Aidha, Jaji Kiongozi mstaafu, Amiri Manento alisema, bila kuwapo kwa haki, amani haiwezi kupatikana hivyo wanapaswa kuwa makini na kuhakikisha amani inadumishwa.
Mjumbe mwingine wa Tume hiyo, Awadh Ally Said alisema katika kipindi hiki, amani ni jambo kubwa linalopaswa kulindwa kwa nguvu zote, kwani licha ya kuwepo kwa viashiria vya uvunjifu wa amani katika nchi za Afrika uchaguzi ni kiashiria pekee cha kuiondoa .

No comments:

Post a Comment