Wafanyabiashara wengi wamekuwa wakilalamikia sana ushindani
kwenye biashara zao. Wengi wamekuwa wakiona ushindani kama kitu ambacho
kinawazuia wao kufikia mafanikio kupitia biashara wanazofanya.
Lakini ukweli ki kwamba ushindani una faida kuliko hasara kwenye
biashara yako. Lakini pia faida hii ya ushindani utaiona kama utakuwa na
misingi sahihi na elimu sahihi ya biashara yako. Kwa kukosa misingi hii sahihi
ushindani utakuwa sumu kwako na utapelekea biashara yako kufa.
Leo kupitia mtandao huu wa NAPENDA BIASHARA, utajifunza faida
tano za ushindani kwenye biashara yako na kama ukiweza kuzitumia vizuri
utaiwezesha biashara yako kukua sana.
1.
Ushindani unaonesha biashara ina wateja.
Faida ya kwanza ya ushindani ni kukuonesha kwamba biashara
unayofanya ina wateja. Kama kusingekuwa na wateja basi hakuna mtu ambaye
angekuwa anafanya biashara hiyo. Kitendo cha kuwepo na wafanyabiashara wengi ni
kiashiria kwamba wateja wapo na hivyo kama ukijipanga vizuri unayo nafasi kubwa
ya kukuza biashara yako.
2.
Kujifunza kutoka kwa wengine.
Unapokuwa kwenye biashara yenye ushindani, unapata nafasi kubwa
sana ya kujifunza kutoka kwa watu wengine ambao wanafanya biashara kama
unayofanya wewe. Katika kujifunza huku utapata mbinu bora sana zitakazoiwezesha
biashara yako kukua. Lakini hii yote ni kama utakuwa tayari kujifunza kupitia
wengine.
3.
Kusukumwa ukue zaidi kibiashara.
Binadamu hatupendi kufanya vitu vigumu mpaka pale inapobidi.
Kama kuna kitu kigumu unatakiwa kufanya utatafuta kila njia ya kukwepa
kukifanya mpaka pale utakapokuwa huna namna nyingine bali ni kufanya. Unapokuwa
kwenye biashara yenye ushindani unalazimika kufikiri zaidi na kuboresha zaidi
biashara yako. Hii ni kwa sababu usipofanya hivyo hutapata wateja kwenye
biashara yako.
4.
Ushindani unaleta ubunifu.
Kama upo kwenye biashara ambayo ina ushindani mkali, kufanya
biashara kama ambavyo kila mtu anafanya au kuwa kawaida itakufanya ushindwe
kupata wateja wengi na hivyo kukosa faida. Ila utakapokuwa mbunifu na kuwapa
wateja kitu cha tofauti, utapata wateja wengi na hatimaye kuongeza faida.
Ushindani utakusukuma wewe uwe mbunifu na ubunifu huu utafanya biashara yako
kuwa bora sana.
5.
Ushindani unaleta huduma bora kwa wateja.
Unapokuwa kwenye biashara yenye ushindani, kuna kitu kimoja
kikubwa kitakachokuwezesha kuendelea kuwepo kwenye biashara, kitu hiko ni
huduma bora kwa wateja. Unapotoa huduma bora kabisa kwa wateja wako unajenga
uhusiano mzuri sana na wateja na hivyo biashara yako kuwa na wateja wa uhakika.
Hii itaisaidia sana biashara yako kukua. Unapokuwa kwenye biashara peke yako ni
rahisi kujisahau na kuanza kutoa huduma mbovu kwa wateja. Lakini ushindani
utakufanya uende hatua ya ziada ya kutoa huduma bora.
Ushindani ni mzuri sana kwenye biashara kama utajua jinsi ya
kuutumia vizuri. Ila kama utaona ushindani ni kitu cha kupambana utaishia
kuondoka kwenye biashara. Chukulia ushindani kwenye biashara yako kama kitu cha
kukufanya uboreshe biashara yako na utoe huduma bora kabisa kwa wateja wako
No comments:
Post a Comment