Thursday 6 August 2015

CUF BADO IPO UKAWA.








CUF IMESEMA INAENDELEA KUBAKI UKAWA LICHA YA LIPUMBA KUJIUZULU
Baada ya Prof Ibrahimu Lipumba kujivua Uenyekiti wa CUF, Chama cha CUF kimesema kuwa kitaendelea kubaki UKAWA na kuulinda umoja huo. Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kaimu Mkurugenzi wa habari, uenezi na mawasiliano kwa umma Ismail Jussa inasema hivi
"Leo tarehe 6 Agosti, 2015 Profesa Ibrahim Lipumba aliitisha mkutano na waandishi wa habari katika Hoteli ya Peacock, mjini Dar es Salaam na kutangaza kwamba amejizulu nafasi yake kama Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Wananchi (CUF).
Sisi kama Chama tumezipokea taarifa hizo na tunayaheshimu maamuzi yake. Ni haki yake ya kikatiba na haki ya kidemokrasia kufanya maamuzi anayoyaona yana maslahi kwake.
Bila shaka, Profesa Ibrahim Lipumba amekifanyia kazi kubwa Chama chetu katika miaka 16 ambayo alikuwa Mwenyekiti wetu, nafasi iliyomfanya awe kiongozi wetu mkuu. Kwa nafasi yake hiyo, pia ametoa mchango mkubwa katika ujenzi wa demokrasia katika nchi yetu. Tunaithamini kazi hiyo na tutaendelea kumheshimu kwa utumishi wake mkubwa kwa Chama chetu na nchi yetu. Tunamtakia kila la kheri katika mipango yake ya baadaye.
Chama Cha Wananchi (CUF) ni taasisi na kinaendeshwa kitaasisi. Ndiyo maana maamuzi yake yote yamekuwa yakifanywa kitaasisi kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Chama. Kwa msingi huo, pamoja na ukweli kwamba kuondoka kwa Profesa Lipumba katika safu ya uongozi kutaacha pengo hasa katika kipindi hichi ambacho tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, tunawahakikishia wanachama na wapenzi wa CUF na wananchi wa Tanzania kwa ujumla kwamba Chama hichi hakitayumba.

No comments:

Post a Comment