Thursday 16 July 2015

KAGAME CUP SOON.

Kwa mujibu wa msemaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto, timu za Al Shandy kutoka Sudan, Al Malakia kutoka Sudan Kusini na KMKM kutoka Zanzibar zinatarajiwa kuwasili leo tayari kushiriki michuano hiyo ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Al Shandy wanatarajiwa kuwasili saa 3:00 asubuhi kwa usafiri wa Shirika la Ndege la Kenya (KQ), wakati KMKM watawasili saa 5:00 asubuhi kwa boti ya Kilimanjaro na Al Malakia wakitatua saa 10 jioni kwa ndege ya Rwanda Air.
Kizuguto alivitaja viwanja vitakavyotumika kwa mazoezi na timu zitakazoshiriki mashindano hayo ni Chuo cha Ualimu (Duce), TCC – Chang’ombe, Sekondari ya Loyola, Bora Kijitonyama, Polisi Kurasini, Chamazi na Uwanja wa Uhuru.
Alisema kuwa timu zitafikia katika hoteli za Durban (Mnazi Mmoja), Chichi (Kinondoni), Ndekha, Grand Villa, Travertine (Magomeni), wakati wenyeji Azam na Yanga nao watakuwa na kambi zao.
Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa KMKM, Ali Bushiri amekunwa na viwango vya wachezaji wake wapya ambao amewasajili kwa ajili ya Kombe la Kagame.
Akizungumza na gazeti hili, Bushiri alisema viwango vya wachezaji hao ni vizuri na kwa hakika watasaidia katika mechi zake za michuano hiyo pamoja na Ligi Kuu ya Zanzibar kwa ujumla.
“Wachezaji hawa watasaidia sana kwa sababu sikukurupuka katika kufanya usajili, nilitulia na kufuatilia. Kumbuka kwamba mimi ni mwalimu wa mpira niliwafuatilia katika michezo mbalimbali na niliporidhika niliwasajili,” alisema. Hata hivyo, aliwataka Wazanzibari wakati kuwaombea dua ili wapeperushe vyema bendera ya Zanzibar.
Wakati huo huo, Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) leo litaendesha mtihani wa utimamu wa mwili kwa waamuzi wa watakaochezesha michuano ya Kombe la Kagame.
Zoezi hilo la utimamu kwa waamuzi watakaochezesha mashindano ya Kagame, litafanyika asubuhi katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kusimamiwa na Kamati ya Waamuzi ya Cecafa.
Waamuzi wanaotarajiwa kuhudhuria zoezi hilo ni Ali Ahmed, Suleiman Bashir (Somalia), Ahmed Djama (Djibouti), Yetayew Belachew (Ethiopia), Kakunze Herve (Burundi), Davis Omweno, Peter Sabata (Kenya), Issa Kagabo, Hakizimana Louis (Rwanda), Ahemd El Faith (Sudan), Lee Okelo na Mashood Ssali (Uganda) na Israel Mujuni na Ferdinand Chacha (Tanzania).

No comments:

Post a Comment